DK. MZURI AONESHA UMUHIMU WA SHERIA BORA ZA HABARI
Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TAMWA ZNZ) Dkt. Mzuri Issa amesema ni muhimu kuwa na sheria bora za habari ambazo zinapelekea kuwepo kwa uhuru wa habari na uhuru wa kujieleza kwa jamii.
Amesema hayo wakati wa mkutano wa kutoa mapendekezo ya marekebisho ya sheria ya tume ya utangazaji ya Zanzibar (No. 7, 1997), ambao uliwashirikisha kamati ya masuala ya habari (ZAMECO), Asasi za kiraia na Tume ya kurekebisha ya Sheria uliofanyika Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Mazizini.
Dkt. Mzuri aliongeza kuwa ipo haja ya kufanyiwa marekesbiso sheria hiyo ili kutoa fursa ya uhuru wa kujieleza ambao ndio chanzo kikuu cha maendeleo ya nchi.
“ Uhuru wa habari na haki ya kupata habari pamoja na uhuru wa kujieleza ni mambo ya msingi katika maendeleo ya nchi na inaleta furaha ya mtu binafsi”, amesisitiza Dkt. Mzuri Issa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa tume ya kurekebisha sheria Zanzibar, Ndugu Khadija Shamte amesema kuwa muda umefika sasa kuwa na sheria zinazokwenda na wakati na tume iko tayari kushirikiana na wadau kwenye kupokea maoni ya kurekebisha sheria ili kutoa fursa kwa vyombo vya habari kukua na kuwa na ushindani katika kusambaza taarifa.
“Tunahitaji kushirikiana kwa pamoja na mwisho kupata sheria bora na nzuri ambayo italeta mabadiliko katika tasnia ya habari Zanzibar”, Khadija Shamte, Mwenyekiti Tume ya Kurekebisha Sheria.
Wakizungumza katika mkutano huo wadau wa habari Zanzibar wamesisitiza tume kuifanyia kazi mapendekezo yote yaliyotolewa na hatimaye kupatikana kwa sheria yenye kukidhi vigezo na inayoikwenda na wakati.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar, Zanzibar Press Club (ZPC), Abdullah Mfaume amesema mapendekezo ya sheria ya habari inarahisisha upatikanaji wa habari katika ukusanyaji, usambazaji wa taarifa kwa waandishi wa habari na itakuwa tija na maslahi kwa jamii.
Ameiomba Tume ya kurekebisha Sheria pamoja na watendaji wengine kuitumia ZAMECO katika kujadili sheria zozote zinazohusiana na masuala ya Uandishi wa habari ili kupata taarifa zaidi kuhusiana na hali halisi na masuala mbali mbali yanayoathiri sekta hiyo.
Mkutano huo wa siku moja unaojadili Sheria zinazohusu habari umeandaliwa na Chama cha Waandishi wahabari Wanawake Tanzania Zanzibar, TAMWA ZNZ chini ya Ufadhili wa Jumuiya ya Madola (Common Wealth.
Comments
Post a Comment