MRADI WA ‘SWIL’ ZANZIBAR, ULIVYOWAONESHA NJIA WANAWAKE KUDAI HAKI ZAO: TAMWA, PEGAO ZASEMA JAMBO
NA HABIBA ZARALI, PEMBA
HAWAKUKOSEA waliosema 'umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu'
Msemo huu umesadiki katika utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wanawake kudai haki zao za uongozi , demokrasia na siasa 'SWIL' unaotekelezwa kwa mashirikiano kati ya TAMWA Zanzibar, ZAFELA na PEGAO.
Mradi huo ambao ulizinduliwa mwaka 2020 na kutarajiwa kumalizika 2023 umeonekana na mafaniko makubwa katika hatuwa mbalimbali za utekelezaji wake.
Utekelezaji wa mradi huo ambao ulitarajiwa kuwafikia na kuwawezesha wanawake 6000 kwa zanzibar, Unguja na Pemba katika kudai haki zao ili nao waweze kuwawezesha wengine tayari umeonyesha njia katika kufikia hatuwa ya kudai haki zao za uongozi.
Mradi huo wa SWIL ambao unafadhiliwa na ubalozi wa Norway umetekelezwa maeneo mbalimbali ambapo kwa upande wa Pemba tayari umeshawafikia wastani wa wanawake 4000.
Katika hatuwa za kufanikisha lengo la mradi la kuwawezesha wanawake kudai haki zao za uongozi demokrasia na siasa kumeanzishwa kamati za Wilaya za kuhamasisha wanawake kudai haki zao za uongozi.
Kamati hizo zinajulikana kwa jina la kiutaalamu 'citizen brigged' asilimia 60 ni wanawake na 40 ni wanaume ambao ndio walengwa wakuu wa kutowa ushirikiano kufikia malengo ya mradi huo.
VIONGOZI WA MRADI
Mkurugenzi mtendaji wa mradi wa Swill kutoka PEGAO Hafidh Abdi Said anasema kwa Wilaya za Pemba mradi umevuuka lengo kwani wameshajengewa uwezo zaidi ya watu waliokusudiwa.
Anasema uhamasishaji huo haukulenga kuwajengea uwezo wanawake hao kuwa viongozi serikalini wala vyama vya siasa pekee bali hadi ndani ya sekta iliyomo ndani ya jamii.
"Wanawake hawatakiwi tu kuingia ndani ya Serikali bali hadi ndani ya vyama, kamati za maendeleo , jumuiya , nafasi za usheha na maeneo mengine",alisema.
Alifahamisha kuwa idadi ya wanawake kwenye uongozi kwa sasa imezidi ukilinganisha na awamu iliyopita Tanzania zanzibar na bara.
Mratibu wa mradi huo kutoka TAMWA Zanzibar Fat-hiya Mussa Saidi anasema tayari mradi umefikia hatuwa ya lengo lililokusudiwa ambapo ndio tarajio lake kwani mradi huu unawawezesha wanawake lakini na wanaume wanahusishwa.
Anaeleza kuwa utekelezaji wao mkubwa ndani ya mradi huo wa swill umewawezsha waandishi wa habari wa Unguja na Pemba, ili wapate uweledi wa masuala ya wanawake na uongozi.
“Tunaamini kama tukiwawezesha vizuri waandishi wa habari watakuwa na maono mapana na kuondokana na dhana zilizo ndani ya jamii juu ya wanawake na uongozi.
Hata hivyo anasema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kufikisha elimu hiyo kwa jamii ,kwani vimekuwa na sauti pana ambayo haifikiwi na taasisi nyengine.
Mapema Mratibu wa mradi huo kutoka PEGAO, Dina Juma Makota anasema wanawake wanapaswa kujiongeza kielimu, washiriki katika masuala ya kijamii, kutokata tamaa, waweze kupambana na kutokana tamaa ili waweze kushinda vikwazo vinavyowekwa na kuwakosesha nafasi za uongozi.
Anasema kupitia mradi huo tayari tayari wamewajengea uwezo wanawake ambao walikuwa hawawezi hata kusimama mbele za watu lakini sasa wanaweza hata hivyo wako walioingia kwenye chaguzi za ndani na kushinda.
Anasema kundi hilo lina haki sawa na la wanaume ingawa wenye mamlaka ,wanaliona tofauti kundi la wanawake ingawa mradi wa kuwawezesha kudai haki zao ‘swill’ unaweza kusaidia kwani hata jamii imeweza kutatuliwa kero ambazo zinawarejesha nyuma”anasema.
WAHAMASISHAJI JAMII KUPITIA MRADI
Nachia Khamis Mohamed wilaya ya Mkoani anasema katika kutembelea vijijini wamebaini changamoto mbalimbali zinazosababisha wanawake wasifikie malengo ya kuwa viongozi ingawa baada ya kugunduwa walilazimika kutowa elimu.
Anasema wamebaini wanawake wengi wanakuwa na lengo la kugombea nafasi za uongozi lakini wanakwazwa ikiwemo ndoa kwani hupambana na wivu kwa wanaume zao, dhana potofu kwa kisingizio cha kuwabadilikia.
Umbali wa skuli kwa baadhi ya maeneo nao unawasababisha kutofika malengo kwani vijana wa kike wengi huishia darasa la tisa na kukatisha masomo jambo ambalo huvisa malengo yao yakiwemo ya kugombea nafasi za uongozi.
“Tunapozikuta chanagamoto zinazowakwaza wanawake kufikia uongozi tunakaa pamoja na kutowa elimu kati ya wanawake na wanaume na kuwaelekeza umuhimu wa mwanamke kuwa kiongozi yote inatokana na dhamira ya mradi wa swil”,anasema.
Ali Abdalla Juma wa wilaya ya Chake chake anasema kutokujiamini ,jamii kuwa na uwelewa mdogo unaohusiana na wanawake na uongozi kwani wengi hawakusoma, wanaume kutowaruhusu wake zao kugombea, mitaji hasa katika nafasi za juu kama ubunge na uwakilishi, ukandamizaji kwa baadhi ya vyama ni mambo yanayofanya wanawake kuwa nyuma katika kugombea nafasi za uongozi.
Baada ya kuona hizo changamoto chini ya mradi huu wa SWIL kwa vile na sisi tumesha wezeshwa basi tuliweza kutowa elimu kwa jamii kwa mifano hai ya kidini na kiulimwengu tukiwahusisha viongozi wa kike akiwemo mama Samia Raisi wa Tanzania pamoja na bi Khadija Binti Khuwailid ambae alikuwa mke wa kiongozi wa kiislamu Mtume Muhammad (S.A.W).
Saada Saleh Ali Wilaya ya Wete anasema kwa upande wao wamegunduwa baadhi ya maeneo wanawake wengi hawajui kusoma na kuandika na tayari wamefanikiwa kuanzishwa kwa darasa la watu wazima katika kijiji cha Kiuyu Minungwini.
“Pamoja na mambo mengine kama vile umbali wa skuli matatizo ya maji ,vituo vya afya vya kujifungulia,ukandamizaji kwa baadhi ya vyama, jamii kutopendana lakini tumefikia hatuwa nzuri ya kuelimisha na ni ukweli usiopingika kuwa kwa sasa kupitia mradi w swill wanawake wameamka”,alisema.
WANAUME
Ali Makame Juma (57) wa Mkoani anasema kabla ya kuja mradi huu wanawake hawakujuwa haki zao na ndio maana ikawa nafasi nyingi zinachukuliwa na wanaume jambo ambalo halikuwa sahihi.
Anasema hatuwa inayochukuliwa na mradi ya kupita katika jamii na kuweza kutowa elimu hiyo ni ya mfano kwa vile wanawake wengi walikuwa wamelala katika suala la kudai haki zao hasa za uongozi na kuwaachia wanaume peke yao.
“Mimi mwenyewe nilikuwa naona kama hakuna umuhimu wa wanawake kuwa viongozi lakini kumbe ni bora tukiwapa wanawake kuongoza kuna neema kubwa kupitia wao kwa vile ni waaminifu kuliko ata sie wanaum
e,”anasema.
Zuhura Juma Khamis (42) wa Chake chake anasema bado wenye mamlaka ambao wengi wao ni wanaume wanawabania kuwapa nafasi wanawake jambo amabalo kwa sasa wanatakiwa kuachana nalo na kuwatizama wanawake kwani nao wanaweza kushika nafasi zaidi ya wanaume.
Salma Suleiman wa Mkanyageni anasema elimu inayotolewa na mradi wa Swill imeweza kuwafunuwa macho wanawake wengi na wameelewa kuwa kumbe kuna fursa mbalimbali wanazikosa kutokana na nafasi nyingi kuchukuliwa na wanaume.
“Sisi huku vijijini ndio ambao tuko nyuma sana hasa katika masuala ya uongozi kwani imezoeleka kuwa mwanamke si wa kuwa kiongozi na badala yake akae nyumbani na kulea watoto basi jambo ambalo limeturejesha nyuma kwa muda mrefu sana.
WANAHARAKATI
Wanaharakati wanaopinga haki za wanawake kisiwani Pemba wanasema wanawake wengi wamekuwa na uthubutu wa kuweza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kuweza kuzikamata.
Tatu Abdalla Msellem anasema hata nafasi za usheha ,udiwani na nyengine katika jumuiya mbalimbali zinaonekana kukamatwa na wanawake jambo ambalo hapo zamani halikuwepo.
Uthibitisho wa hilo ni pale tunapoona kuongezeka idadi ya masheha katika wilaya zilizopo kisiwa cha Pemba, kwa upande wa wilaya ya wete inayo masheha wanawake 14 kati ya shehia 36 jambo ambalo hapo nyuma hawakuwepo.
Wilaya ya chake ambayo ilikuwa na sheha mmoja tu mwanamke sasa imepiga hatuwa hadi kufikia watano ambapo wilaya ya Mkoani nayo imefikia masheha kumi, pamoja na ile ya micheweni iliyofikia masheha nane.
Asha Muhsin Ali anasema lazima wenye mamlaka waone aibu pale wanapowaacha wanawake katika nafasi za uongozi kwa vile wanapopewa nafasi hizo wanaweza kuongoza na kuwashinda hata wanaume.
“Mbona sasa tunaona mabadiliko ya uongozi si haba katika mawilaya ,vyama na hata kamati za maendeleo zilizomo kwenye jamii pakiwa na kiongozi mwanamke hakuharibiki na mambo yote huenda sawasawa”alisema.
VIONGOZI WANAWAKE
Mwakilishi wa jimbo la Chambani Bahati Khamis Kombo anasema mwanamke kushika uongozi ni jambo la neema maana amekuwa mwarubaini wa kumaliza kero.
“Inashangaza na haipendezi hata kidogo kuona kuwa bado wapo wanaume wenye mamlaka hawataki kuwapa wanawake nafasi za uongozi na kuendelea kudidimiza maendeleo yao nay a nchi kwa ujumla”,alisema.
Katibu Tawala Wilaya ya Mkoani Miza Hassan Faki anasema licha ya wanawake kuonekana kuongezeka katika ngazi za maamuzi lakini bado haijaridhisha na inahitaji kuongezeka.
“Mradi huu wa swil una shabaha nzuri kwa jamii na imeonekana kwenye mabadiliko ya wanawake walivyohamasika na kudai haki zao za kuwa viongozi katika sekta mbalimbali na juhudi za mradi huu huenda kwenye uchaguzi 2025 idadi ya wanawake majimboni na kwenye wadi itaongezeka”,alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib anasema ili wanawake wasiweze kuachwa nyuma kwenye nafasi za uongozi jamii itilie nguvu kuwasomesha watoto wa kike ili mwisho wa siku kusiwe na kikwazo cha kielimu ambacho wanakitumia katika kugombea nafasi.
Mkuu wa wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya anasema hakuna tatizo lolote mwanamke kuwa kiongozi ikiwa atajiamini , kufanya kazi zake kwa uweledi na kukusimamia maamuzi aliyoyatowa .
“Mimi apa mwenyewe ni mwanamke na ni kiongozi lakini nafanya kazi zangu bila matatizo yoyote wala siyumbi na napata kuwasemea wanawake wenzangu matatizo yao.
Sheha wa shehia ya madungu Mafunda Hamad Rubea anasema hajaona chanagamoto yoyote ya utendaji kwa kisingizio cha kuwa ni mwanamke kwani muongozo na taratibu za nafasi yake zipo na zimeeleza wazi tena kwa ufasaha.
VIONGOZI WA DINI
Sheikh Said Ahmad Mohamed kutoka ofisi ya Mufti anasema mwanamke hajakatazwa kuwa kiongozi na hasa akiwa atazingatia maadili ,mila na desturi za dini na jamii yake.
“Yapo mambo hupaswa wanawake wajiamulie wenyewe na sio busara kuona mifumo dume inatawala hadi kwa mambo ambayo ni ya pamoja au yanawahusu wanawake pekee,”alisema.
Father Zero Marandu kutoka kanisa katoliki Chakechake anasema hajakatazwa mwanamke kuongoza kwani anasema hakuna kondoo mwanamke kuchungwa na mwanamme , hivyo lazima na wanawake nao wafike kwenye zizi ili kuangalia kondoo wao .
Akimaanisha kuwa mwanamke kuwa kiongozi sio jambo la mjadala maana wenyewe wana ajenda zao wanapaswa wazishughulikie wenyewe.
Ni wakati sasa jamii inapaswa kubadilika na kuacha tabia ya kumuona mwanamke hawezi kuwa kiongozi kwani fikra hizo zinaporomosha maendeleo ya wanawake na jamii nzima hasa ukizingatia wanawake nao wana masuala yao mengi ambayo yanawahusu na yanahitaji kusemewa.
mwisho.
Comments
Post a Comment